Taifa la Kenya leo limeungana na mataifa mengine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukabiliana na Kujitia Kitanzi au kujitoa uhai. Katika maadhimisho haya, wito umetolewa kwa mashirika ya umma na binafsi nchini kuimarisha upatikanaji wa msaada unaohitajika kwa afya ya akili.
Seneta mteule wa chama cha ODM, Hamida Kibwana, akihutubia kwenye hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa kukabiliana na matatizo ya kiakili katika hospitali mbalimbali nchini, alisisitiza umuhimu wa kuyapa kipaumbele masuala ya afya ya akili. Seneta Hamida ameeleza kuwa afya ya akili ni zaidi ya tatizo la kiafya, kwani limegeuka kuwa suala muhimu kwa ustawi wa jamii nzima.
Suala la afya ya akili miongoni mwa viongozi wa kisiasa, maafisa wa polisi na kina mama waliowapoteza wana wao limeangaziwa kwa kina na seneta huyo, akisema kujitia kitanzi hakufai kuwa suala la kisheria bali la kiafya.
Seneta Hamida, akiwa pamoja na wadau wengine kwenye hafla hiyo, alieleza haja ya kutungwa kwa sheria madhubuti ambazo hazitawakandamiza watu wanaokumbwa na changamoto za afya ya akili, na badala yake kuwasaidia kupata msaada unaofaa wa matibabu.
Mwongozo uliozinduliwa hii leo, unapania kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya ya akili katika vituo vyote vya afya nchini. Wizara ya afya pia imezindua mfumo wa mafunzo ya kidijitali ambayo yanaeleza kuhusu matatizo mbalimbali ya akili.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kuwa kila sekunde 40, mtu mmoja hufa kwa kujitia kitanzi. Ulimwenguni, kujitia kitanzi ni sababu ya nne inayoongoza ya vifo kati ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29.