Kesi imewasilishwa mahakamani kupinga matokeo ya KCPE yaliyotolewa na Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) wiki jana. Katika kesi hiyo, wazazi wa mwanafunzi kutoka shule ya Set Green Hill Academy iliyoko Kisii, wanaitaka mahakama kuzuia KNEC kuanza zoezi la usajili wa kidato cha kwanza linalotarajiwa kuanza kesho.

Katika stakabadhi za mahakama, wazazi hao wanahoji kuwa mtahiniwa ambaye pia ni mwanao hakuridhishwi na jinsi karatasi zake zilivyosahihishwa wakidai kuwa matokeo hayo yamemsababishia mtoto wao msongo wa mawazo.

Kulingana na wazazi hao, ikiwa zoezi la usajili litaanza, basi muda wa siku 90 wa mapitio hautakuwa wa busara. Aidha Wazazi na wanafunzi kadhaa nchini wameelezea kutoridhishwa na matokeo yaliyotolewa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu mnamo Novemba 23.

Hata hivyo KNEC ilikiri kuwepo kwa kasoro katika mchakato huo, ikisema kuwa ilipokea rufaa kutokana na makosa ya baadhi ya matokeo yaliyopatikana kupitia nambari ya SMS 40054 ambayo ilitolewa na Wizara ya Elimu.

November 27, 2023