NHIF

Waziri wa Afya nchini Susan Nakhumicha amewasimamisha kazi mameneja wote wa vituo vya Bima ya kitaifa ya Afya NHIF katika maeneo yaliyotajwa kuhusika katika kashfa ya malipo kupitia kwa bima hiyo.

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, waziri Nakhumicha ameeeleza kuwa wizara yake kwa ushirikiano na tume ya kitaifa ya kukabiliana na ufisadi EACC wameanzisha uchunguzi wa kina kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria wote waliohusika katika kuipunja NHIF.

Taarifa yake imejiri saa chache baada ya kutolewa kwa taarifa ya upekuzi kuhusu wizi unaotekelezwa na baadhi ya hospitali za kibinafsi kupitia bima ya NHIF. Waziri huyo pia ameagiza hospitali zilizotajwa kwenye taarifa hiyo kuwatafutia wagonjwa walio katika hospitali hizo matibabu katika hospitali mbadala katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Zaidi ya hayo Nakhumicha ameagiza kuanzishwa kwa uchunguzi wa maisha ya maafisa wote wa NHIF, ili kuhakikisha kwamba wataweza kueleza chanzo cha utajiri wao, huku pia akiiagiza bodi ya NHIF kuanzisha uchunguzi kuhusu sakata hiyo na kuwasilisha ripoti yake katika kipindi cha saa 48 zijazo.

June 19, 2023