Mahakama kuu ya Garsen kutwa ya leo imewapata na hatia ya mauaji maafisa wawili wa polisi waliohusia katika mauaji ya mchungaji wa ngamia katika Kaunti ya Tana River miaka sita iliyopita.
Katika uamuzi wake Jaji Stephen Githinji, amesema kwamba afisa Emmanuel Wanje Mwaringa ambaye ana cheo cha Konstebo wa Polisi, na Afisa Brian Otieno ambaye pia ni polisi wa cheo cha Konstebo katika idara ya Polisi wa Utawala, kwa pamoja walimuua Abdullahi Hussein Omar mnamo Juni 24, 2018 katika Soko la Boka kaunti hiyo ya Tana River.
Uamuzi wa jaji Githinji umeeleza kwamba upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuonyesha maafisa hao walitumia nguvu kupita kiasi kwa kumpiga risasi mchungaji huyo ambaye hakuwa amejihami. Jumla ya wananchi 17 walitoa ushahidi wao kwa faida ya upande wa mashkata kwenye kesi hiyo.