Mgomo

Muungano wa Maafisa wa Kliniki Nchini (KUCO) umesitisha mgomo wake wa kitaifa na kuwaagiza wanachama wake kurejea kazini ndani ya saa 24 baada ya kusaini Makubaliano ya Maelewano (MoU) na Wizara ya Afya pamoja na Baraza la Magavana.

Makubaliano hayo yalisainiwa siku ya Jumatano katika jengo la Afya House katika mkutano ulioongozwa na Waziri wa Afya, Dkt. Deborah Mlongo Barasa, pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana, Gavana Ahmed Abdullahi.

Miongoni mwa matakwa ya maafisa wa kliniki ni pamoja na kutambuliwa rasmi na kujumuishwa kwa watoa huduma na wataalamu waliopata leseni kutoka Baraza la Maafisa wa Kliniki, pamoja na kurejeshwa kwa mamlaka ya kuidhinisha matibabu (pre-authorization rights) kwa maafisa wa kliniki, wakiwemo wale waliobobea, chini ya bodi ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Waziri wa Afya, Dkt. Barasa, aliwapongeza maafisa wa kliniki kwa kukubali kurejea kazini mara moja na kuwataka waendelee kujitolea katika kujenga mfumo wa afya thabiti unaoangazia wagonjwa, ili kuhakikisha huduma bora na nafuu kwa Wakenya wote.

Kwa upande wao, maafisa wa KUCO wakiongozwa na Katibu wa Kitaifa wa muungano huo, George Gibore, na Mwenyekiti wao, Peterson Wachira, wameitaka serikali kuhakikisha kwamba makubaliano haya yanatekelezwa kikamilifu ili kuzuia kurejea tena kwenye meza ya majadiliano.

March 13, 2025

Leave a Comment