Viongozi wa upinzani nchini waliendeleza maandamano ya kushinikiza mabadiliko katika maeneo tofauti ya taifa kwa siku ya kutwa ya leo.
Jijini Nairobi viongozi wa Muungano wa Azimio waliandamana na wafuasi wao katika mitaa mbalimbali, wakiendelea kutoa malalamishi yao na matakwa yao kwa serikali. Hali ilikuwa tulivu kwa sehemu kubwa ya maandamano hayo, kabla ya maafiisa wa polisi kuwatwanya waandamanaji kwa kutumia vitoa machozi nyakati za alasiri walipojaribu kupenyeza katika njia zinazoelekea maeneo ya katikati mwa jiji.
Katika kaunti ya Siaya, maandamano hayo yaligeuka vurumai, lililoshuhudia ofisi za chama cha UDA zikivamiwa na kuteketezwa, huku baadhi ya watu wakiiba mabati yaliyokuwa yameezekwa kama ua katika ofisi hizo.
Hali sawia ilishuhudiwa Katika kaunti ya Kisumu, ambapo biashara nyingi zilisalia kufungwa huku maeneo ya katikati mwa mji yakisalia mahame. Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara wanakadiria hasara baada ya biashara zao kuvamiwa kuibiwa na hata kuharibiwa.
Shughuli za usafiri nazi zilitatizika katika kaunti ya Migori, baada ya wananchi waliojitokeza kushiriki maandamano kufunga barabara kuu ya Isebania-Migori-Kisii. Shughuli za biashara pia zilitatizika pakubwa, maafisa wa polisi wakiwakabili waandamanaji hao.