Serikali imefunga maeneo ya kuuzia pombe 5,995 nchini kote huku msako mkali wa uuzaji wa pombe haramu ukizidi kushika kasi.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Wizara ya usalama wa Ndani ilisema maeneo hayo yalifungwa baada ya kubainika kushindwa kufuata matakwa ya kisheria ya uendeshaji.

Wizara hiyo pia ilibainisha kuwa kufikia sasa Bonde la Ufa limerekodi kiwango cha juu zaidi cha utiifu na kurekodi jumla ya biashara 23,735 zilizoidhinishwa.

Mashariki mwa Kenya ilishika nafasi ya pili ikifuatiwa na mikoa ya Kati, Nyanza, Magharibi, Pwani, na Kaskazini Mashariki. Wizara hiyo iliongeza kuwa asilimia 86 ya maeneo yaliyokaguliwa yamerekodi ufuasi.

Operesheni hiyo ya kitaifa, iliyoongozwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa usalama wa Ndani Kithure Kindiki inalenga kukabiliana na wale wanaouza pombe haramu, na kuendeleza utumizi mbaya wa dawa za kulevya nchini.

Katikati ya mwezi uliopita, serikali ilisema ilikuwa imekamata zaidi ya watu 3,000 sawa na kufunga maeneo 5,000 yasiyokuwa na leseni.

Takwimu za hivi punde kutoka NACADA zinaonyesha kuwa eneo la Magharibi la Kenya linaongoza kwa visa vya ulevi nchinikwa asilimia 23.8%, ikifuatiwa na maeneo ya Pwani na kati kwa asilimia 13.9 na asilimia 12.8% mtawalia.

June 13, 2023