Magavana kutoka kaunti za Nyanza sasa wanaitaka serikali kupeleka maafisa wa Kitengo cha GSU katika mpaka wa Kisumu-Kericho ili kurejesha hali ya utulivu.
Katika taarifa ya pamoja, Magavana Gladys Wanga (Homabay) Ochilo Ayako (Migori) James Orengo, Siaya, na Anyang Nyong’o wa Kisumu wanataka Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuchukua hatua haraka.
Magavana hao wanasema juhudi za polisi kurejesha utulivu katika eneo hilo zimeambulia patupu.Wakuu hao wa kaunti vilevile wanasema mashambulizi katika mpaka huo yameendelea bila kusitishwa tangu Jumatano usiku huku Wakenya kadhaa wasio na hatia wakipoteza maisha na mali.Wanadai suala la mpaka kati ya kaunti hizo mbili pia linafaa kutatuliwa kwa haraka kwa kutumia taratibu halali na mwafaka za serikali.
Kwa upande wao wakaazi wa eneo hilo wamemtaka rais William Ruto kuzungumzia suala hilo kwenye ziara yake ya Nyanza inayoanza wiki hii.