Magavana

Magavana kutoka kaunti mbalimbali nchini wamekongamana katika hoteli ya Keekorok, iliyoko kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Maasai Mara, kwa kikao cha siku mbili kinacholenga kuangazia utendakazi wa serikali zao.

Gavana Ann Waiguru, ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo, ameeleza kuwa kikao hiki kinalenga kuchunguza utendakazi wa serikali za kaunti mwaka mmoja baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa ugatuzi nchini.

Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Gavana Ahmed Abdullahi wa Wajir, ameunga mkono kauli ya Mwenyekiti wake, na kueleza kuwa baraza hilo pia litajadili hali ya mafuriko yaliyoshuhudiwa kaskazini magharibi mwa nchi, ambayo yamesababisha madhara kwa zaidi ya watu 20,000. Mwenyeji wa magavana hawa Gavana Patrick Ntutu wa Kaunti ya Narok, kwa upande wake ameeleza kuwa kaunti yake pia imeathirika kutokana na mvua kubwa, hususan maeneo ya Narok mashariki.

Kikao hiki kinatarajiwa kukamilika hapo kesho, huku Waziri wa Mazingira nchini, Soipan Tuya, akipanga kuongoza baraza hilo katika shughuli ya upanzi wa miti jioni ya leo.

 

November 8, 2023