magavana

Baraza la Magavana limepinga vikali agizo la Mdhibiti wa Bajeti, Dkt. Margaret Nyakang’o, la kusimamisha matumizi ya fedha za kaunti kwa ajili ya basari za wanafunzi. Magavana hao wanasema agizo hilo linawanyima wanafunzi wengi nafasi ya kuendelea na masomo, hali inayozua changamoto kubwa kwa elimu katika ngazi za kaunti.

Kwa mujibu wa magavana, mamia ya wanafunzi wanategemea fedha za basari kutoka kwa kaunti zao ili kuendeleza masomo yao, lakini agizo hilo limekwamisha zoezi hilo. Dkt. Nyakang’o alisisitiza katika agizo lake kwamba jukumu la kufadhili masomo ni la serikali kuu na si la serikali za kaunti.Hata hivyo, magavana wamedai kuwa hawahitaji fedha za ziada kutoka kwa serikali kuu kwa ajili ya mpango huo, na wanasisitiza kuwa hatua ya kuwasaidia wanafunzi haina tatizo lolote.

Baraza la Magavana limeonya kuwa litachukua hatua za kisheria iwapo agizo hilo halitabatilishwa. Pia, magavana hao wamemtaka Dkt. Nyakang’o kuitisha mkutano wa dharura kujadili suala hilo kwa kina na kutafuta suluhisho.

Magavana wanasema wanafunzi wanaotegemea basari hizi hawapaswi kuathirika na mzozo wa majukumu kati ya serikali kuu na serikali za kaunti. Wanasisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi, na kuchelewesha au kusimamisha basari ni kuzuia maendeleo ya wanafunzi hao.

January 21, 2025

Leave a Comment