Jeshi la Taifa litaendelea kusaidiana na maafisa wa polisi katika shughuli za kudumisha amani humu nchini. Hii ni baada ya Mahakama Kuu hapo jana kutoa uamuzi unaoruhusu jeshi kuendeleza shughuli hizo, na kufuta kesi iliyokuwa imewasilishwa na Chama cha Mawakili Nchini (LSK).
Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Mugambi, alieleza katika uamuzi wake kwamba serikali haikuvunja sheria kwa kuwatuma maafisa wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya (KDF) kushika doria ili kuwasaidia maafisa wa polisi kukabiliana na waandamanaji. Hata hivyo, Jaji Mugambi aliitaka serikali, kupitia Wizara ya Ulinzi, kuweka bayana muda ambao wanajeshi watashika doria, maeneo yanayolengwa katika doria hizo, na pia sababu za kutumiwa kwa vikosi vya KDF.
Uamuzi huu unalenga kuhakikisha kuwa shughuli za usalama zinazoendeshwa na vikosi vya KDF zina uwazi na zinazingatia sheria. Hatua hii inakuja baada ya mjadala mkali kuhusu matumizi ya vikosi vya jeshi katika majukumu ya usalama wa ndani, ambao umeibua hisia mseto miongoni mwa raia na wanasiasa. Uamuzi huo pia ulieleza kwamba mahakama ingali na uwezo wa kutoa mwongozo zaidi kuhusu idhini ya wanajeshi katika shughuli zilizotajwa.
Waziri wa Ulinzi Aden Duale kwa upande wake alieleza kwamba wizara yake itafuata maagizo ya mahakama na kutoa maelezo zaidi kuhusu shughuli za KDF.