Mahakama Kuu imesitisha utekelezwaji wa mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu hadi kesi iliyowasilisha mahakamani itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa Oktoba 13, 2023, na Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC), Kikundi cha Elimu Bora, Boaz Waruku, na Baraza la Wanafunzi, inahoji kuwa mfumo huo wa ufadhili ni wa kibaguzi na unawanyima maelfu ya wanafunzi fursa ya kuendeleza masomo yao katika vyuo vikuu.
Jaji Chacha Mwita katika uamuzi wake alisema kuwa kesi hiyo itatajwa Desemba 16, 2024. Mfumo huo uliozinduliwa Mei 3, 2023 na Rais William Ruto unanuiwa kujumuisha usawa katika kufadhili wanafunzi wa vyuo vikuu na TVET kupitia mseto wa ufadhili wa masomo na mikopo.
Kwingineko Chuo kikuu cha Moi kimefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia mgomo wa muda mrefu wa wahadhiri na wafanyakazi wengine wa chuo hicho, ambao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa mishahara na kutotekelezwa kwa mkataba wa CBA.
Wafanyakazi hao zaidi ya 4,000 wamegoma kwa takriban mwezi mmoja.
Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Isaac Kosgey, alisema katika notisi kwamba bodi ya chuo kikuu cha Moi imeazimia kusimamisha shughuli zote za masomo na ufundishaji za muhula wa 1 katika mwaka wa masomo wa 2024/2025 kutokana na mgomo huo.