Mahakama ya juu nchini Imewazuia wakenya wanne walioteuliwa na Rais William Ruto katika Baraza la Kitaifa la Mabadiliko ya Tabianchi (NCCC) dhidi ya kutwaa wadhifa huo, hadi pale kesi iliyowasilishwa dhidi yao itakapoamuliwa.
Jaji Mugure Thande mapema leo alitoa Maagizo ya kusitisha uteuzi wa Emily Mwende Waita, John Kioli, Umar Omar na George Odera Outa katika baraza hilo, akieleza kuwa kesi iliyowasilishwa na walalamishi kadhaa ilifikia kiwango hitajika cha kuwezesha kusitishwa kwa uteuzi wao.
Kupitia kwa wakili Henry Kurauka walalamishi hao ambao ni pamoja na Mt Kenya Network Forum na Indigenous People National Steering Committee on Climate Change walitilia shaka zoezi la uteuz huo wakisema kwamba umma haukuhusishwa inavyofaa kabla ya kufanyika kwa uteuzi huo.
Pia walieleza kuwa uteuzi wa Rais unakiuka mwongozo wa sheria za baraza hilo ambazo zinatoa nafasi kwa watu kutoka mashirika kadhaa kuhudumu.