Seoul, Korea Kusini – Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini imethibitisha uamuzi wa Bunge wa kumbandua madarakani Rais Yoon Suk Yeol, ikihitimisha utawala wake na kufungua njia kwa uchaguzi mpya wa rais ndani ya miezi miwili.
Katika hukumu iliyotangazwa moja kwa moja kwenye runinga za kitaifa, Jaji Mkuu wa muda wa mahakama hiyo, Moon Hyung-bae, alisema kuwa Yoon alitangaza sheria ya kijeshi kinyume cha Katiba na sheria za nchi kwa kutumia vikosi vya jeshi na polisi kuzuia mamlaka ya Bunge kutekeleza majukumu yake. Mahakama ilieleza kuwa tangazo hilo lilikiuka vigezo halali vya kutangaza hali ya hatari na liliathiri utawala wa kikatiba kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa mahakama, athari hasi za uamuzi wa Yoon zilikuwa kubwa kiasi kwamba kulinda Katiba kwa kumuondoa madarakani kulionekana kuwa muhimu zaidi kuliko faida yoyote ambayo ingeweza kupatikana kwa kumwacha aendelee kuongoza.
Katika taarifa kupitia timu yake ya utetezi, Yoon alisema kuwa anajutia kushindwa kuafikia matarajio ya umma lakini hakusema moja kwa moja kama anakubali uamuzi wa mahakama. Alieleza kuwa kuhudumia taifa ilikuwa heshima kubwa zaidi maishani mwake.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wake, Yoon Kap-keun, alikosoa uamuzi huo kwa kusema kuwa haukuwa wa haki na kwamba ulikuwa uamuzi wa kisiasa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Han Duck-soo, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa muda wa taifa, aliahidi kuwa hakutakuwa na pengo katika masuala ya usalama wa kitaifa na diplomasia, huku akisisitiza kuwa serikali itahakikisha usalama wa umma na utulivu wa kitaifa unadumishwa.
Huku uchaguzi wa rais ukitarajiwa kufanyika ndani ya miezi miwili, wachambuzi wa siasa wanasema kuwa mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kuhusu kuondolewa kwa Yoon unaweza kuathiri juhudi za Korea Kusini katika kushughulikia sera za “America First” za Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na uhusiano wa Korea Kaskazini na Russia.