MAHAKAMA YA MILIMANI

Mahakama kuu nchini imedinda kutoa agizo la kusitisha zoezi la mchujo wa shule za upili kwa wanafunzi waliokamilisha mtihani wa KCPE mwaka huu.

Katika uamuzi wake siku ya Jumatano, Jaji Lawrence Mugambi wa Mahakama Kuu ya Milimani ameamuru kwamba kesi zilizowasilishwa kuhusu matokeo ya KCPE zisikizwe Februari 7, mwaka ujao. Aidha walalamishi katika kesi hiyo wametakiwa kuwasilisha malalamishi yao kwa wizara ya elimu katika kipindi cha siku 14 zijazo.

Siku ya Jumatatu 27 Novemba 2023, wazazi wawili kutoka shule ya Kitengela International Academy na ile ya Set Greenhill Academy, waliwasilisha kesi mahakamani wakipinga matokeo ya KCPE yaliyotangazwa na waziri Eliud Machogu Alhamisi iliyopita, wakidai kuwa kulikuwa na makosa katika mfumo wa uwekaji alama.

SOMA PIA: Kesi yawasilishwa mahakamani kupinga matokeo ya KCPE yaliyotolewa wiki jana.

Hapo awali Baraza la mitihani ya kitaifa  KNEC lilikiri kuwepo kwa kasoro katika matokeo, ikisema kuwa ilipokea rufaa kutokana na makosa ya baadhi ya matokeo yaliyopatikana kupitia nambari ya SMS 40054 ambayo ilitolewa na Wizara ya Elimu.

November 29, 2023