Mahakama ya Nairobi imeondoa kesi ya jinai dhidi ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na washtakiwa wengine sita.
Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kutuma maombi ya kutaka kesi hiyo iondolewe, baada ya uamuzi wa mahakama kuu uliotangaza shtaka la kupindua sheria kuwa kinyume na katiba.
Babu alikamatwa wakati wa maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali yaliyoidhinishwa na muungano wa Azimio la Umoja.
Alishtakiwa pamoja na Calvine Okoth Otieno almaarufu Gaucho, Tom Ondongo Ong’udi, Michael Otieno Omondi, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino Baraka.
Mbunge huyo amesema kuwa ataelekea mahakamani kuwasilisha ombi la kulipwa fidia kwani haki zao zilikiukwa. Wakihutubia wanahabari baada ya uamuzi wa mahakama, mawakili wake Danstan Omari na Duncan Okatch walisema kwamba kuna uhuru wa kujieleza na kuandamana na ni jukumu la serikali kuheshimu kifungu cha 37 cha katiba.