BY ISAYA BURUGU,20TH NOV,2023-Mahakama Kuu imetoa uamuzi wa kusitisha agizo la serikali la kutaka baadhi ya maafisa wa polisi 67 kusimamishwa kazi kwa madai ya kupokea hongo na makosa mengine.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei Alhamisi wiki jana alimwagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kuwasimamisha kazi maafisa hao kutokana na pendekezo la Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi.
Lakini maafisa hao walienda kortini kusimamisha agizo hilo wakitaja ukiukaji wa taratibu za kinidhamu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi.
Kupitia kwa wakili Danstan Omari, walitaka maagizo ya kusitishwa kwa agizo la Koskei wakisema lingekiuka pia haki yao ya kuchukuliwa hatua za kiutawala kwa kuwa hata hawakufahamishwa kuhusu uamuzi wa kuwasimamisha kazi.Jaji Chacha Mwita, baada ya kusoma maombi hayo, alikubali maagizo hayo.
EACC imeorodheshwa kama mhojiwa wa kwanza huku Koskei akiwa mjibu wa pili. Mahakama iliagiza kesi hiyo kusikizwa mnamo Novemba 23 kwa maelekezo zaidi.