Makenzi

Mhubiri maarufu anayehusishwa na utoaji wa mafunzo ya kupotosha katika msitu wa Shakahola, Paul Makenzi, ataendelea kusalia gerezani kwa muda zaidi. Hii leo, upande wa mashtaka leo uliwasilisha ombi mahakamani kutaka mhubiri huyo na washukiwa wenzake wazuiliwe kwa siku 180 zaidi ili kuendeleza uchunguzi.

Makenzi alifikishwa mahakamani ya Shanzu siku ya Jumatatu, lakini kesi yenyewe haikusikilizwa. Wakili Wycliffe Makasembo, ambaye ni wakili wa utetezi, alisema kwamba hawako tayari kwa vikao vya kesi hiyo kwa sababu pande zote zinazohusika hazijapata nyaraka zote zinazohitajika ili kuanza kesi.

SOMA PIA: Mawakili waliokuwa wakimwakilisha Paul Mackenzi wajiondoa.

Hii leo, Mahakama iliamua kuweka tarehe mpya ya kusikiliza kesi hiyo, ambayo itakuwa Oktoba 12, na kuagiza upande wa mashtaka kuhakikisha kwamba kila upande unaohusika unapata nyaraka zinazohitajika kwa kesi hiyo.

Mhubiri huyo alitiwa nguvuni mwezi Aprili, baada ya kugunduliwa makaburi ya halaiki katika eneo la Shakahola. Inadaiwa kwamba mhubiri huyo aliwashinikiza wafuasi wake kufunga kula na kunywa hadi kuaga dunia. Maafisa wa idara mbalimbali za usalama wamekuwa wakiendesha shughuli za kuwatafuta manusura. Tangu kutiwa nguvuni, zaidi ya miili 429 imepatikana katika makaburi ya pamoja kwenye Msitu wa Shakahola.

Makenzi amekaa rumande kwa takriban miezi mitano bila kufunguliwa mashtaka, huku akiwa anakabiliwa na mashtaka yasiyopungua 12. Mashatka haya ni pamoja na mauaji, ugaidi, kusaidia mauaji, utekaji nyara, mauaji ya halaiki, ukatili dhidi ya watoto, utapeli na pia utakatishaji fedha.

September 18, 2023