Manusura 65 waliookolewa kutoka eneo la Shakahola waliokua wakipokea huduma za matibabu siku ya Jumatatu walifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka la kukusudia kujitoa uhai kwa kukataa kula, katika Kituo cha uokoaji cha Sajahanadi huko Mtwapa.
Manusura hao walisomewa shtaka hili baada ya kufikishwa katika mahakama ya shanzu, huku upande wa mashtaka ukiomba manusura hao kuhamishwa hadi katika jela ambapo kuna nafasi itakayowawezesha kuepuka msongamano katika kituo hicho cha uokoaji. Sitini na tano hao hata hivyo hawakukukubali au kupinga mashtaka, huku mahakama ikiamuru wafanyiwe vipimo vya akili na pia kulazimishwa kula.
Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Shanzu Joe Omido anatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu kesi hiyo tarehe 15 mwezi huu.
Siku ya leo miili 10 zaidi imefukuliwa kutoka katika eneo hilo la shakahola, kwenye zoezi la awamu ya tatu ya ufukuzi unaoendelea sasa, huku shughuli za kuwatafuta manusura zaidi zikishika kasi. Hadi kufikia sasa, idadi jumla ya watu walioaga dunia katika eneo hilo imefikia 284 huku watu wengine 613 wakiwa hawajulikani waliko na wanshukiwa kuwa walihusika katika matukio kwenye msitu huo.
Wakati hayo yakijiri, kamati ya uchunguzi iliyotwikwa jukumu la kuangazia matukio katika eneo la Shakahola, mapema leo ilikutana na wawakilishi wa baraza la viongozi wa kiislamu nchini SUPKEM na Baraza la Wahindu, ili kupokea maoni kuhusu mtazamo wao katika matukio ya Shakahola.
Katika kikao hicho, SUPKEM iliibua maswali mengi kuhusiana na jinsi washukiwa katika kesi hii waliendeleza shughuli zao bila maafisa wa polisi kutambua, na pia hatua madhubiti zinazofaa kuchukuliwa kwa watu wanaoendeleza mafunzo ya itikadi kali humu nchini.