Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa mataifa yanayoshiriki kwenye Kongamano la Umoja wa Mataifa la Bayoanuai – COP 15 nchini Canada kushiriki katika jukumu la dharura la kufikia makubaliano thabiti ya kulinda viumbe hai duniani.
Akizungumza mjini Montreal kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kilele, Guterres amesema ulimwengu unapigana vita na mazingira ya asili, na kwa hiyo kongamano hilo lina jukumu la dharura la kutengeneza amani.
Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau aliyatolea wito mataifa yanayoshiriki kuilinda asilimia 30 ya ardhi zao na bahari ifikapo mwaka wa 2030 ili kusitisha uharibifu wa viumbe hai.
Wajumbe wa mkutano huo wana matumaini kuwa mkutano huo wa kilele wa wiki mbili, unaojulikana kama COP15, utahakikisha ulimwengu unasalia kuwa na viumbe asilia kama wanyama, mimea na mifumo mizuri ya ikolojia ifikapo 2030, kuliko ilivyo sasa.