Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa na Ujerumani wako mjini Addis Ababa kwa lengo la kuunga mkono makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana kumaliza miaka miwili ya vita vikali.
Ziara ya Catherine Colonna wa Ufaransa na Annalena Baerbock na Ujerumani imjiri siku moja baada ya waasi wa Tigray kutangaza kuwa wanaanza kusalimisha silaha zao nzito, ikiwa ni kipengele muhimu cha muafaka wa Novemba 2 wa kusitisha mapigano kaskazini mwa Ethiopia.
Wakati wa ziara yao ya siku mbili, mawaziri hao watakutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na mawaziri wengine pamoja na maafisa wa Umoja wa Afrika na wanaharakati wa haki za binadamu, na kukitembelea kituo cha usambazaji wa chakula cha Shirika la Umoja wa Mataifa.
Taarifa ya kidiplomasia imesema mawaziri hao wanapeleka ujumbe kutoka kwa Umoja wa Ulaya kuwa uko tayari kushirikiana upya na Ethiopia mradi mpango wa usitishwaji mapigano unaheshimiwa.