Vita vya ubabe kati ya wawakilishi wadi wa kunti ya Meru na gavana wa kaunti hiyo Bi. Kawira Mwangaza vimeonekana kuchukua mkondo tpfauti, baada ya wawakilishi wadi hao kukataa kuwaidhinisha mawaziri 7 kati ya 10 waliopendekezwa na gavana huyo.
Katika orodha ya uteuzi, wawakilishi wadi waliyaidhinisha majina ya mawaziri wateule watatu pekee ili kutwaa nyadhifa za uongozi katika uongozi wa kaunti hiyo. Wawakilishi wadi wa kaunti hiyo wamekuwa wakizozana peupe na gavana kawira mwangaza kuhusiana na maswala ya marupurupu na pia utendakazi wa gavana huyo.
Mawaziri walioidhinishwa ni Pamoja na Monica Kathono – Wizara ya fedha/Hazina ya Kaunti, Thuranira Ithana – Maswala ya Elimu, na Dickson Mûnene – Maswala ya kisheria. Hatua hii itamlazimu gavana Kawira Mwangaza kufanya upya uteuzi wa mawaziri na kuwasilisha orodha nyingine katika bunge la kaunti kwa ajili ya kupigwa msasa.
Gavana Kawira Mwangaza alionekana kulegeza msimamo wake dhidi ya wawakilishiwadi hao, hasa baada yake kuwaalika katika kikao cha kuzungumzia maswala yao na kujaribu kutatua mgogoro unaoshuhudiwa kati ya gavana na wawakilishiwadi hao.