Kamati ya uteuzi katika Bunge la Kitaifa leo itaendesha vikao vya kuwapiga msasa mawaziri watatu walioteuliwa kujiunga na Baraza la Mawaziri. Mawaziri hao ni aliyekuwa Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe (Kilimo), pamoja na magavana wa zamani William Kabogo (Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali) na Lee Kinyanjui (Biashara).
Kwa mujibu wa ratiba, Mutahi Kagwe atakuwa wa kwanza kufika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge Moses Wetangula, kuanzia asubuhi. Kabogo atafuata mwendo wa saa tisa alasiri, huku Lee Kinyanjui akifunga vikao mwendo wa saa kumi na moja jioni.
Mawaziri hao waliteuliwa na Rais William Ruto mnamo tarehe 19 mwezi uliopita, na iwapo uteuzi wao utaidhinishwa na Bunge, watachukua nafasi rasmi za majukumu yao. Kabogo, atachukua nafasi ya Margaret Nyambura, ambaye aliondolewa katika baraza la Mawaziri.
Uteuzi huu unatafsiriwa kama hatua ya kuimarisha uhusiano wa kikazi kati ya Rais Ruto na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta. Mawaziri hawa wote ni washirika wa karibu wa Uhuru.
Katika mabadiliko mengine, Kipchumba Murkomen aliteuliwa Waziri wa Usalama wa Ndani, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Kithure Kindiki, ambaye sasa ni Naibu Rais. Salim Mvurya alihamishiwa Wizara ya Vijana na Uchumi wa Ubunifu.