Semi za kisiasa zilitawala hafla ya mazishi ya Shujaa wa Mau mau Bi. Mukami Kimathi hii leo, wanasiasa waliohudhuria wakitumia muda walipata mbele ya kipaza sauti kuvuta ngoma upande wao.
Kati ya vigogo waliopata nafasi ya kuzungumza ni Pamoja na Kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga ambaye aliwarai viongozi wakuu serikalini kushughulikia gharama ya juu ya Maisha, na kujiepusha na kuwaongezea wakenya mzigo wa Ushuru.
Aidha viongozi wa serikali waliohudhuria hafla yenyewe kwa idadi zao, walikariri mmoja baada ya mwingine kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu uliokamilika, wakimtaka Bw. Odinga kukubali matokeo ya uchaguzi na kuiopa serikali nafasi ya kutekeleza ajenda yake ya maendeleo.
Kwa upande wake, Rais William Ruto aliendelea kutetea serikali yake, akiahidi kuendelea kurekebisha uchumi na kuyatatua matatizo yanayowahangaisha wakenya. Rais hakusita kujibu kauli za Odinga, akieleza kwamba utawala uliopita uliboronga uchumi wa taifa kwa kuwekeza katika kutoa ruzuku kwa matumizi badala ya kuboresha uzalishaji.