Mazungumzo ya maridhiano kati ya mrengo wa Azimio la Umoja na Kenya kwanza yatatekelezwa kwa kipindi cha siku sitini kuanzia Alhamisi tarehe 11 mwezi Mei.
Hii ni baada ya pande zote zinazohusika katika mazungumzo haya kukubaliana kuhusu mambo ya msingi yatakayo jadiliwa katika vikao vya Pamoja. Katika taarifa iliyotolewa baada ya kikao kilichodumu kwa sehemu kubwa ya kutwa ya leo.
Viongozi wa pande zote mbili ambao wanaongoza mazungumzo haya Otiende Amollo na Seneta Boni Khalwale wameeleza kuwa mambo yenye utata Zaidi yatajadiliwa ya kwanza katika kipindi cha siku 30 za kwanza kabla ya kuendelea kwa mazungumzo kuhusu maswala mengine yaliyo kwenye orodha ya maswala ya kujadiliana.
Baadhi ya masuala yaliyopendekezwa na mrengo wa Azimio ni Pamoja na suala la kushusha gharama ya Maisha, Ukaguzi wa matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022, mchakato wa kuunda upya Tume ya IEBC huku mrengo wa kenya kwanza ukipendekeza kujadiliwa kwa masuala kuhusiana na kuundwa upya kwa jopo la uteuzi wa Makamishna wa IEBC, Kanuni ya kijinsia ya thuluthi mbili, kuanzishwa kwa Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Eneobunge (NG-CDF) Pamoja na Kuundwa kwa Ofisi ya Kiongozi Rasmi ya Upinzani.