Mbunge wa Sirisia John Waluke amejisalimisha kwa polisi baada ya mahakama kuu kuidhinisha kifungo chake cha miaka 67 gerezani kutokana na ulaghai wa shilingi milioni 297.
Haya yanajiri saa 24 baada ya Jaji Esther Maina kutupilia mbali rufaa yake, na kuamua kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha.Kulingana na Jaji Maina, mashtaka hayo yalithibitishwa pasipo shaka yoyote na hukumu hiyo si ya kupindukia ikizingatiwa kwamba iko ndani ya sheria.
Mshtakiwa mwenza wa Waluke, Grace Wakhungu, alitiwa mbaroni hapo jana baada ya uamuzi huo na kwa sasa anazuiliwa katika Gereza la Wanawake la Lang’ata.Mbunge huyo aliwasilisha hati yenye vipengele 30 mnamo Juni 2020, kupitia kwa mawakili wake, akielezea kile alichokiita kutofautiana na ukosefu wa uhuru katika kufikia uamuzi wa hatia.
Pia alipinga hukumu yake, akidai ilitokana na hati ya mashtaka isiyo sahihi.Hukumu ya Waluke ilijiri kufuatia kesi ya ufisadi ambapo alishtakiwa kwa kuilaghai Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) shilingi milioni 313.
Mbunge huyo alishtakiwa pamoja na Grace Sarapay Wakhungu, na Erad Supplies & General Contracts Limited kampuni ambayo wawili hao ni wanahisa.
Waluke na Wakhungu, kupitia kampuni hiyo, walipaswa kusambaza tani 40,000 za mahindi kwa NCPB mwaka wa 2004 lakini wakaishia kuweka mfukoni fedha hizo bila kusambaza mahindi kwenye bodi hiyo.Zabuni hiyo hata hivyo ilifutiliwa mbali baada ya kampuni ya Erad Supplies, ambayo marehemu mfanyabiashara Jacob Juma pia alikuwa mkurugenzi, kukosa kuthibitisha ilikuwa na pesa za kutosha kusambaza mahindi hayo.
Kampuni hiyo baadaye ilielekea kortini na kuishtaki NCPB ikidai kuwa wakati zabuni hiyo ilifutwa, tayari ilikuwa imenunua mahindi hayo kutoka Ethiopia na kwamba yalikuwa yakihifadhiwa na Chelsea Freight, kampuni ya Afrika Kusini, nchini Djibouti.