Mchungaji Ezekiel Odero sasa ataweza kufikia akaunti zake zote za benki ambazo zilikuwa zimefungiwa kwa siku 15. Hii ni baada ya kukamilika kwa siku 15 zilizotolewa na mahakama.

Afisa mpelelezi Inspekta Martin Munene akiwa anahojiwa na Wakili Danstan Omari, aliambia mahakama kwamba kutokana na hati iliyopokelewa hakuna akaunti yoyote iliyokuwa na jina la Ezekiel.

Alisema akaunti zote ni za kanisa au shule.Hata hivyo, afisa huyo alisema Safaricom haijatii agizo la mahakama kufikia leo na kutaka waitwe kwa kutotoa data zinazohusiana na kadi za simu za mchungaji huyo.

Kesi hiyo itatajwa Jumanne wiki ijayo ili kuthibitisha ikiwa Safaricom itakuwa imetii agizo la mahakama.

Omari pia alifahamisha mahakama kuwa mteja wao Mchungaji Ezekiel kwa sasa yuko katika kanisa lake la Mavueni ambapo wakuu wa usalama na wakili Cliff Ombeta wanapitia katika majengo yake ili kuthibitisha masuala.

May 22, 2023