Mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake watazuiliwa kwa siku 30 zaidi  huku maafisa wa upelelezi wakichunguza mauaji ya Shakahola, ambapo zaidi ya watu 133 hadi sasa wamethibitishwa kufariki.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Yusuf Shikanda ambaye alisema kuwaachilia huru kwa washukiwa hao kutahatarisha usalama wao pamoja na upelelezi unaoendelea.

Aidha upande wa mashtaka ukiongozwa na Jami Yamina, uliotaka washukiwa hao kuzuiliwa kwa angalau siku 90, ulionyesha kutoridhishwa na muda uliotolewa na mahakama.

Mhubiri huyo alikuwa miongoni mwa washukiwa wengine 17, akiwemo mkewe, ambao walifikishwa katika mahakama ya Shanzu hii leo.

wakati hayo yakijiri makanisa ya Good News International na New Life Prayer Center, yanayomilikiwa na wahubiri wenye Paul Mackenzie na Ezekiel Odero mtawalia yamepokea notisi za kughairiwa kutoka kwa Msajili wa mashirika.

Kulingana na Maria Goretti Nyariki, Naibu Msajili wa mashirika, kanisa la Mchungaji Mackenzie, lilipokea notisi ya siku 30 ya sababu ya kutofuata sheria.

Bi Nyariki aliambia Kamati ya muda inayoongozwa na Seneta Mungatana kuhusu mauaji ya Shakahola kwamba kanisa la Mackenzie lilikuwa likitii sheria tangu kusajiliwa kwake 2010, hadi 2022, wakati jaribio la kubadilisha jina lilipofanywa.

Mackenzie pia alikuwa ajiuzulu kama mwenyekiti wa kanisa hilo.

May 10, 2023