Gavana wa kaunti ya Narok Patrick Ntutu ameahidi kubuni kamati maalum ya watu 30 itakayokuwa na jukumu la kusuluisha mizozo kati ya wanyama pori na binadamu katika mbuga ya kitaifa ya Maasai Mara.
Ntutu ambaye alikua akizungumza katika eneo la sekenani siku ya Ijaumaa 21.10.2022, alisema kuwa wakati umewadia siasa kuwekwa kando katika maswala ya kuilinda mbuga ya kitaifa ya Maasai Mara. Gavana huyo amesema kuwa ukame unaoshudiwa kwa sasa umesabisha wafugaji kuingia katika mbuga hiyo kutafuta lishe ya mifugo wao hatua ambayo imesababisha ongezeko la idadi ya visa vya uhasama kati ya wanyama pori na binadamu.
Katika hotuba yake,gavana Ntutu amesema kamati hiyo itaangazia hatua za wenyeji wa eneo hilo kukabiliana na wanyama pori kila kukicha na kutafuta suluhu la kudumu, huku akiongeza kuwa serikali yake imetenga fedha zaidi ili kuinua viwango vya maendeleo eneo hilo. Taarifa ya gavana Ntutu inajiri siku kadhaa baada ya kisa cha ndovu kutoka mbuga hiyo ya Maasai Mara kuvamia baadhi ya wananchi katika maeneo jirani.