Moto Narok

Gavana wa Kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu, ameahidi kuanzishwa kwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha mkasa wa moto uliotokea katika kituo cha uchukuzi wa magari mjini Narok. Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, Gavana Ntutu alifichua kuwa tayari kulikuwepo na onyo kwa wafanyabiashara dhidi ya kutumia mitungi ya gesi katika maduka yaliyopo kwenye eneo hilo.

Adhuhuri ya jana, mkasa wa moto unaodaiwa kusababishwa na mlipuko wa gesi ya kupikia ulisababisha hasara kubwa baada ya kuteketeza maduka mawili kabla ya juhudi za kuzima moto kufanikiwa. Tukio hilo limeibua mjadala mkali miongoni mwa wafanyabiashara wanaohisi kuwa hatua za kudhibiti usalama zinahitajika kwa haraka.

Baadhi ya wafanyabiashara walioshuhudia mkasa huo wanasema moto ulisambaa kwa kasi na kuharibu mali katika duka la simu, hoteli, na kinyozi. Wafanyabiashara hao wanakadiria hasara kubwa na kuimarishwa kwa uwezo wao wa kukabiliana na majanga kuepusha tukio jingine kama hilo.

Gavana Ntutu aidha ameahidi kuwa serikali yake itachukua hatua zinazofaa kuhakikisha usalama wa wafanyabiashara na wananchi katika maeneo ya umma mjini Narok.

January 9, 2025

Leave a Comment