Kindiki

Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof. Kithure Kindiki, amelaani vikali ghasia zilizotokea katika eneo la Sondu, kwenye mpaka wa kaunti za Kericho na Kisumu, siku ya Jumatano. Waziri Kindiki ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vilivyotokea na idadi kubwa ya majeruhi waliopatwa katika makabiliano hayo.

Akizungumza katika soko la Sondu baada ya kufanya mkutano wa usalama katika mikoa ya Rift Valley na Nyanza, Waziri huyo amesema kuwa ghasia hizo zilipangwa na wahalifu ambao walitumia mgogoro wa mipaka kama kisingizio. Aidha, ameongeza kuwa vitendo hivyo vya uhalifu na ukatili havitavumiliwa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

Akizungumzia mandamano yaliyoitishwa na mrengo wa upinzani juma lijalo, Waziri Kindiki amewaonya wale wote wanaokusudia kusababisha uharibifu wa mali za Wakenya wenzao na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi. Kindiki amesisitiza kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi ya wahalifu hao na watajutia vitendo vyao, akisema kwamba wana haki ya kushiriki maandamano, iwapo watayafanya kwa njia ya amani.

 

 

July 15, 2023