Gavana wa Narok Patrick Ntutu, Waziri wa mazingira Soipan Tuya Pamoja na Waziri wa Utalii Penina Malonza, wameongoza shughuli za uzinduzi wa mpango wa usimamizi wa mbuga ya maasai mara kutwa ya leo.

Viongozi hao wamekariri kujitolea kwa idara zao kuendelea kutunza mbuga hiyo. Gavana Ntutu amesema uzinduzi wa mpango huo utasaidia katika ukuaji wa sekta ya utalii nchini na pia katika taifa jirani ya Tanzania. Gavana huyo aidha ameeleza kuwa mchakato wa kuidhinisha mipango hii ulikosa kueleweka inavyofaa na wananchi wengi na hata viongozi, ila amesema kuwa manifaa yake yataonekana wazi katika siku za usoni.

Waziri Malonza amekashifu maandamano ya upinzani akisema kuwayanahitilafiana na shughuli za utalii katika sehemu mbalimbali humu nchini, akisema kuwa hatua ya kuwa na maandamano imepelekea watalii kuhofia kutembea mbuga hiyo. Waziri huyo amesema mbuga kitaifa ya Maasai Mara ni dhahabu katika ukuaji wa kiuchumi na pia katika sekta ya utalii nchini kenya na katika ukanda wa Africa mashariki. Zaidi ya hayo, Malonza amepongeza jamii ya maa nchini kwa kuifadhi tamaduni zao kwa miaka.

Kwa upande wake waziri wa mazingira nchini Soipan Tuya amesema serikali haitamsaza yeyote anayeparamia na kuvamia msitu wa Mau. Soipan amesema serikali itaweka ua kikamilifu katika msitu huo, ili kuzuia uharibifu wa mara kwa mara.


Viongozi wengine waliohudhuria hafla hii wanajumuisha katibu mkuu wa utalii nchini John Oloontua, katibu mkuu wa wanyama pori Sylvia Museyia, katibu mkuu wa tamaduni Umi Bashir,naibu gavana wa Narok Tamalinye Koech, mbunge wa Africa mashariki David Sankok, seneta wa Kajiado Lenku Seki, mbunge wa Narok kusini Kitilai Ntutu na pia mbunge wa Kilgoris Julius Sunkuli.

March 23, 2023