Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ametetea safari za Rais William Ruto nje ya nchi. Akihutubia wanahabari alipokuwa akielezea mafanikio ya serikali, Mwaura alisema Kenya imepata manufaa ya thamani ya Ksh.2 trilioni kutokana na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Ruto ametia saini tangu kutwaa madaraka mwezi Septemba mwaka jana.
Alitaja uwekezaji ambao Kenya imepokea kutoka kwa mataifa kama vile Uingereza, Marekani na Uchina. Kulingana na msemaji huyo wa serikali, Rais ametia saini Mkataba wa kibiashara, nishati, usafiri, elimu, kazi na usalama, na kufungua nchi kwa fursa za biashara.