Katika uamuzi uliotolewa mapema leo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisii, Bi. Christine Ogweno, mshukiwa mkuu katika kisa cha unyama kilichoelekezwa kwa Mtoto Junior Sagini mwishoni mwa mwaka jana amehukumiwa kifungo cha miaka 40 gerezani. Kisa hiki kilichotokea katika Kijiji cha Ikuruma, Kaunti ya Kisii kiligusa nyoyo za wengi na kushtua taifa nzima.

Mshukiwa huyo, Bwana Alex Maina, ambaye ni binamu ya Mtoto Junior Sagini, alipatikana na hatia ya kuhusika moja kwa moja katika tukio la kinyama ambapo macho ya mtoto huyo yalitolewa. Hukumu hii imetolewa baada ya kesi yenyewe kukawia mahakamani tangu mwezi Disemba mwaka jana, huku pia ikibadilishwa kutoka kwa kesi ya kukusudia mauaji hadi kesi ya Kusababisha madhara ya kimwili.

Wahusika wengine wawili katika kesi hiyo, ambao ni shangazi wa mtoto Sagini, Bi. Pacifica Nyakerario, na nyanyake, Bi. Rael Mayaka, wamehukumiwa vifungo vya miaka 10 na miaka 5 mtawalia kwa kuhusika kwao katika kisa hicho.

Hakimu Bi. Christine Ogweno alitoa uamuzi huo baada ya kesi hiyo kufuata taratibu zote za kisheria na kufanyiwa uchunguzi wa kina. Uamuzi huu unatoa matumaini kwa familia ya Mtoto Junior Sagini na jamii kwa ujumla, kwamba haki imetendeka na wahusika wa kitendo hiki cha unyama wamekabiliwa na matokeo ya vitendo vyao vya kikatili.

 

 

July 24, 2023