Mwalimu aaga dunia Garissa

Mwalimu mmoja katika kaunti ya Garissa ameaga dunia asubuhi ya Jumanne, baada ya kugongwa kichwani na kipanga (Propeller) ya helikopta iliyokuwa ikisafirisha mtihani wa KCSE. Tukio hilo limetokea eneo la Masalani huko Ijara, wakati wa usamabazaji wa mitihani katika vituo mbalimbali.

Kamishna wa Kaunti ya Garissa, Solomon Chesut, amethibitisha kisa hicho cha kusikitisha, akisema kwamba bado haijabainika alichokuwa akifanya mwalimu huyo karibu na helikopta hiyo iliyokuwa ikitaka kupaa, kabla ya kugongwa na kufariki papo hapo. Kulingana na baadhi ya waliokuwa katika eneo la mkasa, Mwalimu huyo alikuwa na haraka ya kuabiri ndege hiyo ili kuendeleza shughuli za kusambaza mitihani katika vituo mbalimbali kwenye kaunti ndogo ya Ijara.

Matumizi ya ndege za helikopta katika usambazaji wa mitihani ya kitaifa kwenye kaunti ya Garissa yamekuwa ni hatua ya dharura kutokana na hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na uharibifu wa barabara nyingi katika kaunti hiyo. Serikali imekuwa ikilenga kuhakikisha kuwa mitihani inawafikia wanafunzi licha ya changamoto za hali ya hewa.

 

November 21, 2023