Mtihani wa Kidato cha Nne KCSE umeanza rasmi kwa watahiniwa wote asubuhi ya leo katika vituo mbalimbali vya mitihani katika kote nchini. Katika kaunti ya Narok, zoezi hili limeanza katika vituo 189 na watahiniwa wapatao 14,544 waliosajiliwa wanatarajiwa kufanya mtihani huu.

Naibu Kamishna wa Narok ya Kati, Kennedy Mwang’ombe, ametoa hakikisho la usalama kwa watahiniwa wote wanaofanya mtihani huu. Mwang’ombe ameeleza kwamba maafisa wa polisi wamepata mwongozo wa kutosha ili kuhakikisha kuwa zoezi hili linakwenda vizuri. Katika maeneo yanayoshuhudia mvua kubwa, idara ya usalama imeweka tayari maafisa na magari ya kutosha ili kukwamua dharura yoyote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Narok, Apollo Opuko, ameeleza kwamba hakuna kisa chochote cha mwanafunzi anayefanya mtihani huu akiwa mja mzito kimeripotiwa hadi sasa. Hata hivyo, kuna mwanafunzi mmoja anayefanya mtihani hospitalini baada ya kuugua jana usiku. Zaidi ya hayo, wasimamizi wa vituo 201 na waangalizi 667 watasimamia mtihani katika kaunti ya Narok.

SOMA PIA: Waziri wa Elimu apinga madai ya wizi wa mtihani wa KCSE mwaka jana.

Nchini Kenya, jumla ya watahiniwa 903,260 wanafanya mtihani wa Kidato cha Nne KCSE mwaka huu. Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa KNEC, Dkt. David Njeng’ere, ameonyesha imani katika uadilifu wa mtihani huu, hususan kwa mfumo wa kukusanya karatasi za mtihani mara mbili kwa siku. Dkt. Njeng’ere alizindua kasha la mitihani katika Kaunti ya Kiambu asubuhi ya leo.

November 6, 2023