Waziri wa usalama nchini Kithure Kindiki ameeleza kwamba taifa la kenya litafanikiwa katika vita dhidi ya wizi wa mifugo na ujambazi unaotekelezwa katika maeneo ya kaskazini mwa bonde la ufa.
Akizungumza katika kikao kwenye bunge la seneti alipojiwaisilisha ili kutoa majibu kwa maseneta, Kindiki amesema kwamba taifa la Kenya limepiga hatua kubwa katika kukabiliana na uhalifu huu, huku akiongeza kwamba shughuli za wahalifu hawa zimeanza kuchukua mkondo wa kuwa na itikadi kali kama za kigaidi, na wala sio shughuli ya kitamaduni tena.
Katika taarifa sawia, mkuu wa baraza la mawaziri nchini Musalia Mudavadi alihudhuria vikao vya bunge la kitaifa hii leo, ili kutoa taarifa kuhusu mipango ya serikali kuboresha gharama ya Maisha nchini, na jinsi shughuli nzima inaendelea kutekelezwa.
Mudavadi aliorodhesha baadhi ya mipango ambayo serikali imechukua ili kuhakikisha kwamba wakenya hawataendelea kuumia kutokana na gharama ya juu ya Maisha, ikiwemo utoaji wa mbolea yenye ruzuku kwa wakulima kote nchini katika kipindi kilichopo cha upanzi.
Mkuu huyo wa Mawaziri pia amesema kwmaba taifa lilishuhudia kupungua kwa mazao na hasa mahindi nchini kutokana na kipindi cha ukame, idadi ya mahindi yaliyozalishwa ikipungua hadi mifuko milioni 34 kutoka kwa mifuko milioni 50 inayozalishwa kila mwaka.