Muhammad Yunus, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, ameteuliwa kuongoza serikali ya mpito ya Bangladesh baada ya Sheikh Hasina, kujiuzulu na kuikimbia nchi hiyo kufuatia maandamano makubwa yaliyoongozwa na wanafunzi wa vyuo vikuu ya kupinga utawala wake.
Yunus, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Hasina, ataongoza serikali hiyo ya mpito hadi uchaguzi mpya utakapofanyika. Uamuzi wa kumteua Yunus ulifikiwa katika mkutano uliowahusisha viongozi wa maandamano ya wanafunzi, wakuu wa kijeshi, wawakilishi wa asasi za kiraia, na viongozi wa wafanyabiashara.
Waandamanaji wamesema hawatakubali serikali inayoongozwa na jeshi, na wameongeza kuwa Yunus amekubali kuwa mshauri mkuu wa serikali ya mpito. Moja ya masharti yaliyotolewa na waratibu wa maandamano ya wanafunzi ilikuwa kuvunja Bunge, na kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya rais, Bunge la Bangladesh lilivunjwa siku ya Jumanne, ili kutoa nafasi kwa uchaguzi mpya.
Hivi sasa, jeshi limechukua udhibiti wa taifa hilo, huku hatua za kuandaa uchaguzi mpya wa kumpata waziri mkuu zikitarajiwa kuanza.