Hakuna taifa linaloweza kupiga hatua za maendeleo bila kuwa na mfumo unaofaa wa kukusanya ushuru. Haya ni kwa mujibu wa waziri mwandamizi nchini Musalia Mudavadi, ambaye amewasuta wanaokosoa mapendekezo yaliyo katika mswada wa fedha wa 2023/24 akiwataka kutoa mapendekezo mbadala ya jinsi taifa litaweza kukusanya ushuru.
Mudavadi ambaye alikuwa akizungumza mchana wa leo katika ukumbi wa KICC alipokutana na wanachama wa chama cha kitaifa cha wafanyabiashara na wenye viwanda nchini, amesema kwamba uchumi wa taifa la Kenya umekuwa ukitaabika kutokana na uchache wa watu wanaolipa ushuru.
Waziri huyo ameeleza haja ya wakenya kujitolea katika kuendeleza taifa la Kenya, huku akiwataka wale wanaopinga mswada wa fedha, kutoa mapendekezo mbadala ya jinsi taifa litaweza kuimarika.