Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umejitokeza kwa mara nyingine na kudai kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 mwaka jana Raila Odinga, alishinda kinyang’anyiro hicho mbele ya mshindani wake wa wakati huo na ambaye sasa ni rais William Ruto.
Katika kikao na waandishi wa Habari, katibu mkuu wa kitaifa wa Chama cha Jubilee Jeremiah kioni alidokeza kuwa Bwana Odinga alishinda uchaguzi huo kwa kujizolea kura 8,170,355 ambazo ni asilimia 57.53 ya kura zote zilizopigwa, huku Rais William Ruto akijizolea kura 5,915,973 ambazo ni sawa na asilimia 41.66 ya kura zote.
Kioni ameeleza kuwa wametumia ripoti mfichuzi kutoka katika tume ya IEBC, Pamoja na taarifa ya uchunguzi wa mashirikia yasiyo ya kiserikali.
Zaidi ya hayo, Kioni ameeleza kuwa kulikua na shughuli ya kuhitilafiana na matokeo katika maeneobunge mengi hasa katika ukanda wa mlima Kenya, huku akiahidi kuwa muungano huo utatoa taarifa zaidi katika siku zijazo.