Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umetoa wito kwa Wakenya kujiunga na vuguvugu la ‘sufuria movement’ kuanzia kesho ambapo maandamano ya kupinga serikali yatafanyika kwa siku tatu mfululizo.
Akizungumza katika ofisi za Wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga siku ya Jumanne, kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua alisema kuwa vuguvugu hilo litaashiria upungufu wa chakula katika taifa, ambao umesababishwa na gharama ya juu ya maisha.
Wakati huo huo, ametoa wito wa kuwasilishwa kwa picha zozote zilizorekodiwa zinazonasa aina yoyote ya ukatili wa polisi ulioshuhudiwa katika maandamano ya wiki jana kwa nia ya kuwafikisha mahakamani.
Kinara wa wiper Kalonzo Musyoka kwa upande wake amedai kuwa dhamira ya kikosi maalum cha OSU ni aidha kuwaua au kuwadhuru viongozi wa Azimio na Wakenya wakati wa maandamano.