RUTO ON GACHAGUA

Rais William Ruto amefichua matukio yaliyochangia kuondolewa ofisini kwa aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua. Rais alisema kuwa hali hiyo ilitokana na mizozo ya ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

Katika mahojiano na wanahabari usiku wa Jumatatu, Ruto alieleza kuwa mvutano ulianza baada yao kuingia madarakani. Gachagua aliingia katika migogoro na wandani wa rais wakiwemo mwanablogu Dennis Itumbi, Mbunge Ndindi Nyoro, na Kiongozi wa Wengi Bungeni Kimani Ichung’wah. Rais alieleza kuwa alishangazwa na mizozo hiyo na hakuelewa sababu yake.

Kwa mujibu wa Ruto, Gachagua alitaka wabunge wamtii bila pingamizi. Hata hivyo, wabunge walihisi kulazimishwa, hali iliyosababisha uhasama kati yao. Hatimaye, walichukua hatua ya kumwondoa madarakani kwa kumbandua.

Rais pia alikanusha kuhusika moja kwa moja na uamuzi huo, akisisitiza kuwa mchakato wa kisheria ulifuatwa kikamilifu. Aidha, Ruto alifichua kuwa Gachagua alidai kima cha Shilingi bilioni 10 ili kuhakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya linaunga mkono uongozi wake. Hata hivyo, Rais alikataa shinikizo hilo, akisema kuwa hatokuwa tayari kutoa fedha hizo hata ikiwa itamfanya kuwa rais wa muhula mmoja.

Licha ya hali ya kisiasa, Ruto alipuuzilia mbali hofu kuhusu ziara yake ya kaunti tisa za Mlima Kenya inayoanza hii leo. Ziara hiyo inalenga kuwaeleza wananchi kuhusu maendeleo ya serikali yake.

April 1, 2025

Leave a Comment