Mwanaharakati wa haki za binadamu aliyepuliza kipenga kuhusu kashfa ya madai ya ubadhirifu wa Bima ya kitaifa ya Afya NHIF sasa anasema maisha yake yamo hatarini.
Salesio Thuranira, mkazi wa kaunti ya Meru, hivi majuzi alifichua jinsi wagonjwa kadhaa walio katika mazingira magumu na ambao wamejiandikisha kwa NHIF, walipoteza maelfu ya pesa zilizonyakuliwa na makampuni yanayofanya kazi kwa ushirikiano na hospitali za kibinafsi kupitia mikataba isiyofaa ambayo ni pamoja na mfumuko wa bei ya matibabu.
Thuranira anadai kuwa siku chache baada ya sakata hilo kuwekwa hadharani kupitia vyombo vya habari, alipokea vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana na kulazimika kuishi mafichoni.
Ameripoti kisa hicho kwa polisi na anataka usalama wake na familia yake sawa na uchunguzi uharakishwe.