Mwanamke

Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 24 katika Kaunti ya Narok, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kumnajisi mvulana wa miaka 15. Mary Yamati Njoki alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Narok, Phillis Shinyada, ambapo alihukumiwa kwa kosa hilo.

Njoki alipatikana na hatia ya kumnajisi mvulana huyo mnamo tarehe 4 Januari mwaka jana katika eneo la Fanaka, Kaunti Ndogo ya Narok ya Kati. Mwanadada huyo alikamatwa tarehe 21 Januari 2023 na kuzuiliwa huku kesi ikiendelea mahakamani. Alishtakiwa kwa makosa mawili: kumnajisi mtoto mdogo na kushiriki ngono na mtoto mdogo.

Hata hivyo, mwanamke huyo alikuwa amekana mashtaka hayo, lakini mahakama ilimpata na hatia baada ya mashahidi watano kutoa ushahidi wao. Katika harakati za kujitetea, Njoki aliomba mahakama kumhurumia akisema ana watoto wawili ambao wanamtegemea.

Katika uamuzi wake, Hakimu Phillis Shinyada alisema kwamba wazazi wanapaswa kuwa walinzi wa watoto na sio wenye kuwadhulumu. Aidha, alisisitiza kwamba kesi ya dhuluma za kingono haina adhabu ya faini.

July 18, 2024