BY ISAYA BURUGU 18TH FEB,2023-Mwanasoka wa Ghana Christian Atsu amepatikana amefariki chini ya vifusi vya nyumba yake nchini Uturuki takriban wiki mbili baada ya tetemeko la ardhi kukumba nchi hiyo na kusababisha majumba mengi kuporomoka.

Ajenti wa mchezaji huyo, Murat Uzunmehmet amethibitisha kuwa mwili wake hatimaye umepatikana kufuatia shughuli ya utafutaji wa kina ya zaidi ya siku 10.

Christian Atsu, aliyekuwa mchezaji wa Chelsea.
Image: HISANI

Murat alisema kwamba baadhi ya vitu vya mwanasoka huyo wa miaka 31 pia zilipatikana chini ya vifusi hivyo.

Mwili wa Atsu usio na uhai ulipatikana chini ya vifusi. Hivi sasa, vitu zaidi bado vinatolewa. Simu yake pia ilipatikana,” alisema.

Ajenti Nana Sechere alifariji familia ya marehemu na kuwashukuru wote waliosaidia katika shughuli ya utafutaji.

“Mwili wa Christian Atsu umepatikana asubuhi ya leo. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wote kwa maombi yao na usaidizi,” aliandika.

Raia huyo wa Ghana alitoweka baada ya tetemeko la ardhi lenye kipimo cha 7.8 kutokea nchini Uturuki alfajiri ya Februari 6.

Alikuwa ameratibiwa kuondoka saa chache kabla ya tetemeko hilo, lakini meneja wa Hatayspor alisema  Mghana huyo aliamua kusalia na klabu hiyo baada ya kufunga bao la kufutia machozi katika mechi ya Februari 5 ya Super Lig.

Atsu ambaye alikuwa akichezea klabu ya Uturuki, Hatayspor kabla ya kukumbana na kifo chake cha kuhuzunisha aliwahi kuwakilisha klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza zikiwemo Chelsea, Everton na Newcastle.

Zaidi ya watu 42,000 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika tetemeko hilo la ardhi lililotokea mapema mwezi huu.Mamilioni ya watu pia wameachwa bila makao baada ya nyumba zao kuporomoka.

February 18, 2023