Mauaji Narok

Wananchi wa maeneo ya Total na K24, viungani mwa mji wa Narok, waliandamana siku ya Alhamisi, kulalamikia mauaji ya mwanaume mmoja yaliyotokea usiku wa Jumatano katika eneo la K24.

Maandamano hayo yalisababisha kusitishwa kwa muda shughuli za kawaida kwenye barabara kuu ya Narok kuelekea Bomet. Wakazi hao wanalalamikia utepetevu wa maafisa wa usalama baada ya ongezeko la visa vya majambazi wanaowavamia nyakati za usiku.

Kulingana na taarifa kutoka idara ya usalama, mwanaume huyo, ambaye alikuwa saveya wa Kibinafsi, alivamiwa na watu wasiojulikana karibu na lango la kuingia nyumbani kwake majira ya saa tatu usiku.

Kamishna wa kaunti ya Narok, Isaac Masinde, amethibitisha tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi umeshaanzishwa ili kuwakamata wote waliohusika na tukio hilo la kinyama. Aidha, amewasihi wananchi kuwa watulivu na kuwapa idara ya usalama nafasi ya kufanya uchunguzi.Tukio hili la hivi karibuni linajumuishwa katika orodha ya visa vingi vya utovu wa usalama Narok Mjini, ambavyo vimeongezeka hasa kuelekea mwisho wa mwaka jana.

Mwenyekiti wa usalama katika bunge la kitaifa, Gabriel Togoyo, ambaye pia ni mbunge wa Narok Magharibi,alitoa risala za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuhakikisha kuwa hatua zitachukuliwa kuhakikisha usalama wa wananchi wa Narok.

 

January 11, 2024