Mwanaume mwenye umri wa miaka 50 amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kukiri kumoa msichana mwenye umri wa miaka 9.
Saigulu Ololosereka aliyefikishwa katika mahakama ya Narok mbele ya hakimu mkuu Phyllis Shinyada alishtakiwa kwa mashtaka mawili yakiwemo kumnajisi msichana wa miaka tisa pamoja na kumoa mwaka wa 2019.
Katika hukumu yake, Bi. Shinyada alieleza kuwa Ololosereka alionywa kuhusu uzito wa kesi hiyo baada yake kukiri kufanya makosa hayo ila alishikilia kuwa alimuoa msichana huyo ikizingatiwa kwamba wazazi wake walimuoza akiwa na umri huo mdogo.
Kando na hayo, mahakama iliamuru wazazi wa msichana huyo kutiwa mbaroni kwa kosa la kumlazimisha aolewe licha ya umri wake mdogo.
Hali kadhalika upande wa mashtaka ulionyesha kuridhishwa na hukumu hiyo huku mshukiwa akipewa muda ya siku 14 kukata rufaa katika mahakama kuu iwapo hajaridhishwa na hukumu hiyo.