BY ISAYA BURUGU 15TH AUG 2023-Mwananchi  mmoja amewasilisha ombi mbele ya Bunge la Kitaifa la kupiga marufuku mtandao wa kijamii wa TikTok humu nchini .Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula ametangaza kwamba Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Bridget Connect Consultancy Bob Ndolo amewasilisha ombi hilo kutokana na maudhui kwenye jukwaa hilo.

Kulingana na mwombaji, mtandao huo wa kijamii unakuza vurugu, maudhui ya ngono ya wazi, matamshi ya chuki, lugha chafu na tabia za kuudhi miongoni mwa vijana.Amezidi kulalamika kuwa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) haijasimamia jukwaa na mambo yanazidi kwenda kombo.

Ndolo aidha ameongeza  kuwa kutokana na ukosefu wa udhibiti na tabia ya uraibu ya programu, huenda nchi ikashuhudia kushuka kwa ufaulu wa masomo na kuongezeka kwa masuala ya afya ya akili miongoni mwa vijana.

Mwombaji alidai kuwa TikTok hukusanya kiasi kikubwa cha data kwa watumiaji wake ikiwa ni pamoja na maelezo kuhusu kifaa chao, eneo na historia ya kuvinjari, na kuishiriki na makampuni mengine bila idhini ya watumiaji.

 

 

August 15, 2023