Mwili Papa

Mwili wa Papa Francis umehamishwa rasmi kutoka kwenye Chapel ya Mtakatifu Marta hadi kwenye Basilika ya Mtakatifu Petro, mjini Vatican. Waamini wanapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho kabla ya mazishi yake, yaliyopangwa kufanyika Jumamosi.

Shughuli hiyo ilianza kwa ibada fupi ya kiliturujia iliyofanyika Jumatano asubuhi, ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Ibada hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano wa Baraza la Makadinali, ambao tayari walikuwa wameanza kukusanyika mjini Roma kufuatia kifo cha Papa Francis kilichotokea Aprili 21.

Ibada hiyo iliongozwa na Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma. Katika hatua ya mwanzo, alianza sala ya ufunguzi katika nyumba ya Mtakatifu Marta. Katika sala hiyo, alimshukuru Mungu kwa huduma ya miaka 12 ya marehemu Papa Francis na kumuombea apumzike kwa amani ya milele.

Baada ya hapo, maandamano rasmi ya kuleta jeneza yalianza kutoka Uwanja wa Mtakatifu Marta. Yalipitia chini ya Tao la Kengele na kuingia kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, kama ilivyopangwa katika ratiba ya Vatican.

Wakati huo huo, zaidi ya waamini 20,000 walikusanyika katika uwanja huo. Walitoa heshima zao kwa kupiga makofi ya heshima wakati jeneza lilipokuwa likibebwa kuelekea kanisani. Jeneza liliwekwa mbele ya madhabahu ya juu ndani ya basilika hiyo.

Katika mazingira hayo ya ibada na ukimya wa heshima, kwaya iliongoza waamini kuimba Litania ya Watakatifu kwa lugha ya Kilatini. Aidha, Kardinali Farrell aliendeleza Liturujia fupi ya Neno. Usomaji wa Injili ulitoka katika kitabu cha Yohane (17:24-26), ambapo Yesu anasali kwa ajili ya wanafunzi wake na kueleza upendo wa Mungu unaomiminika kwao kupitia yeye.

Ibada hiyo imekuwa sehemu ya mfululizo wa matukio ya kumuaga Papa Francis. Matukio haya yanatarajiwa kuendelea hadi siku ya mazishi yake. Hadi sasa, waamini kutoka kote duniani wanaendelea kumiminika Vatican kwa heshima na maombi ya mwisho kwa kiongozi huyo aliyegusa maisha ya wengi kwa unyenyekevu na mafundisho ya amani.

MAELEZO YA ZIADA KUTOKA KWA VATICAN NEWS

April 23, 2025

Leave a Comment