Ajali ya Barabarani Narok

Naibu Kamanda wa Polisi wa Narok, Calvins Ochieng Onganda, amefariki katika ajali ya barabarani iliyotokea mapema leo katika eneo la Ratili kwenye barabara kuu ya Narok – Bomet.

Kulingana na ripoti ya Idara ya Usalama, ajali hiyo ilitokea wakati gari lake aina ya Toyota Premio, lilipokuwa katika harakati za kulipita lori lililokuwa mbele yake, liligongana uso kwa uso na lori aina ya Hino lililokuwa likitokea upande wa Narok kuelekea Bomet.

Afisa huyo wa polisi alipata majeraha mabaya kwenye miguu yote miwili na kifuani na kufariki dunia papo hapo. Mwili wa marehemu tayari umepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Longisa kwa ajili ya kuhifadhiwa ikisubiri uchunguzi wa maiti.

Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Narok, Bwana Riko Ngare, amethibitisha taarifa za ajali hii, akiongeza kuwa uchunguzi zaidi unafanywa kuhusu ajali hiyo. Magari yenyewe pia yamepelekwa katika kituo cha polisi cha Ololulung’a kwa uchunguzi zaidi.

March 25, 2024